Monday 15 February 2016

NILIPOFANYA KILIMO CHA MATIKITI MAJI KWA MARA YA KWANZA

Sehemu ya tano(mwisho)

UVUNAJI WA MATUNDA

Baada ya siku sabini tulisitisha umwagiliaji katika shamba letu kwa muda wa wiki moja kabla ya uvunaji,hii inasaidia kufanya matunda yajitengenezee sukari na kuyafanya kuwa matamu zaidi,pia inasaidia kuepusha kupasuka kwa matunda.Huu ni ushauri ambao tulipewa na Bwana shamba.
Baada ya siku sabini na tano(unaweza kuenda mpaka siku themanini)shamba letu lilikuwa tayari kwa ajiri ya kuvuna na tulianza shughuli ya uvunaji.
Kilichonishangaza na kunifurahisha ni kwamba siku ya uvunaji nilipata kampani kubwa sana kuliko kipindi chote,karibu kijiji kizima kilikuja kunisaida kuvuna,watoto kwa wazee.

                                          vijana wakivuna matikiti maji shambani



picha za juu,vijana wakipakia matikiti maji kwenye gari tayari kwa kupeleka sokoni


SOKO
Wakati wa kuvuna mazao yetu walikuja wafanyabiashara mbalimbali kutaka kununua mazao yote.Hawa jamaa kwa kawaida humpunja mkulima ili wao wapate faida kubwa zaidi(mpaka mara tatu au nne ya bei waliyonunulia).Hivyo sisi tulikuwa tumejipanga kuuza wenyewe sokoni.Tulikodisha canter mbili tukasomba mzigo wote na kuupeleka katika soko la Buhongwa ambalo ni karibu zaidi.Tuliomba nafasi kwenye uongozi wa soko na kuweka bidhaa zetu na kuanza kuuza kwa jumla na rejareja na mimi mwenyewe nikiwa msimamizi mkuu.Kwavile kulikuwa na uhaba wa matikiti maji sokoni kwa kipindi hicho tuliweza kumaliza mzigo wetu ndani ya wiki moja tu na mauzo yetu yalikuwa ni jumla ya shilingi millioni nane.Gharama zote nilizotumia hazikufika millioni moja.Hivyo basi nilitengeneza shillingi millioni saba kwa muda wa miezi mitatu tena kwa kilimo nilichokifanya kwa mara ya kwanza na pasipo uzoefu wowote.
KAMA UNATAKA MALI UTAYAPATA SHAMBANI.

Tuesday 9 February 2016

NILIPOFANYA KILIMO CHA MATIKITI MAJI KWA MARA YA KWANZA

SEHEMU YA NNE

palizi ya pili na uwekaji wa mbolea

Baada ya mwezi mmoja na wiki mbili mimea na nyasi zisizohitajika vilikuwa vimeshaota hivyo ulikuwa ni wakati muafaka wa kufanya palizi kwa mara ya pili.Tulipalilia lakini pia tuliweka mbolea kwenye mimea yetu na safari hii sikuweka mbolea za madukani bali nilitumia mbolea ya samadi iliyooza vizuri.
                                          Nikishiriki kikamilifu zoezi la uwekaji wa mbolea


Wadau wakiweka samadi katika mitikiti maji.

Katika hatua zote hizi shughuli ya umwagiliaji ilikuwa ni ya kila siku,pia zoezi la upuliziaji wa madawa lilikuwa likiendelea na tulikuwa tukipulizia dawa mara moja kwa wiki.

MBOLEA YA MAJANI

Katika kipindi hiki pia tulitembelewa na bwana shamba ambae alitupatia ushauri wa kuanza kutumia mbolea ya kunyunyizia kwenye majani ya mimea yetu,mbolea hizi lengo lake ni kurutubisha jani la mmea na tunda,na katika hatua hii matunda yalikuwa yameshaanza kutokeza kwa wingi.kwa kawaida zipo aina nyingi za mbolea za namna hiyo japo sisi tulitumia NPK,hii inapatikana katika mfumo wa unga unga hivyo unapaswa kuichanganya na maji kwa kutumia maelekezo stahiki na kunyunyiza kwenye majani.

Matunda machanga katika mimea
Mdau akinyunyiza mbolea ya majani katika mimea

Tuliendelea kufuatilia mimea yetu kwa karibu sana na tulipogundua tatizo lolote tuliwahi kulitatua kwa kufuata ushauri wa kitaalamu.Nilijifunza mambo mbalimbali kupitia kwenye mitandao pamoja na kufuata ushauri wa wataalamu(mabwana na bibi shamba) na baada ya miezi miwili shamba letu lilikuwa linapendeza na lilibeba matunda ya kutosha na yenye afya nzuri kabisa











Thursday 4 February 2016

NILIPOFANYA KILIMO CHA MATIKITI MAJI KWA MARA YA KWANZA

SEHEMU YA TATU

Palizi ya kwanza na uwekaji wa mbolea

Katika sehemu hii ya kilimo chetu shughuli kubwa ilikuwa utunzaji wa shamba letu ambapo kazi kubwa ilikuwa kumwagilia mimea,kupulizia dawa.Kikubwa zaidi shughuli ya palizi ya kwanza ilianza rasmi,kwa vile mimea ilikuwa na wiki tatu hivyo majani yasiyohitajika yalikuwa yameanza kumea karibu na mimea yetu.Kazi ya palizi iliendana na uwekaji wa mbolea .
Tulitumia mbolea aina ya NPK kwa ajiri ya kukuzia mimea,japo katika hatua hii nilitembelea wakulima wengine na kukuta kila mmoja ana formula yake ya aina gani ya mbolea itumike katika hatua hiyo.Baadhi walitumia samadi iliyooza vizuri na wengine walitumia KANI,.sisi tulitumia NPK.

                                Mdau akipalilia palizi ya kwanza katika shamba la tikiti maji

                                           Mdau akiweka mbolea aina ya NPK baada palizi

  Baada ya uwekaji wa mbolea tuliendelea na umwagiliaji wa mimea yetu na baada ya wiki moja tena mimea yetu ilikuwa imekuwa kwa kiasi kikubwa na kuanza kutambaa.
                                        Mdau akipulizia dawa ya kuua wadudu katika mimea.


Ningependa kuwaeleza wasomaji mbalimbali wa makala hii kuwa,ukizingatia matumizi ya dawa za ukungu na wadudu katika kilimo cha matikiti maji utakumbana na changamoto chache sana.japo kuna changamoto zingine ni za mazingila husika kama vile hali ya hewa.mfano kuna maeneo mimea inaathiliwa sana na ukungu au utitili,hivyo matumizi ya dawa yanapaswa yawe ni ya mala kwa mala.
Picha zifuatazo hapo chini ni kati ya madhara ya wadudu katika matikiti maji...

                                            mmea ulioshambuliwa na wadudu waharibifu



                              Mmea ulioshambuliwa na utitiri mweusi ambao hukaa chini ya tawi

Kwa kawaida mimea iliyoathilika kwa kiwango hicho hapo juu inanafasi ya kuambukiza mimea mingine,Hivyo ni bora mkulima akiwa anapulizia dawa mala kwa mala ili kuepuka athali hizo,lakini pia mimea hiyo inaweza kupona kama ikipata huduma ya madawa




Tuesday 26 January 2016

SEHEMU YA PILI

Hatua ya pili

Katika hatua hii tulianza rasmi kulinda mimea yetu dhidi ya wadudu na magonjwa mbalimbali,na mbaka muda huo tulikua tunajua adui zetu wakubwa ni ukungu pamoja na utitiri(mwekundu au mweusi),hivyo tulinunua madawa ya ukungu pamoja na madawa ya kuua wadudu wanaoweza kushambulia mimea yetu.Tulikuwa tukipulizia dawa ya ukungu mara moja kwa wiki na hata dawa ya wadudu(sumu)tulipulizia mara moja kwa wiki.Lakini hizi dawa hazikutumika kwa wakati mmoja,sumu ya wadudu ilitumika peke yake kwa wakati wake(siku tofauti)na dawa ya ukungu ilitumika tofauti kwa wakati wake.Wakati huo huo kazi ya umwagiliaji iliendelea kama kawaida.
mdau akinyunyizia dawa ya ukungu kwenye mitikiti

CHANGAMOTO!!

Mimea iliendelea vizuri sana mpaka nikawa najipa moyo kuwa kulimo hiki nimekipatia kwelikweli mpaka pale changamoto halisi zilipoanza kujitokeza,na hapo ndipo nilipogundua wengi hukata tamaa na kilimo.Ilikuwa ni wiki moja tangu mimea yetu ichipue na ilikuwa ni yenye afya nzuri kabisa.Nikiwa nazungukia shamba nikagundua mimea mingi sana ikiwa imekatwa na kubaki shina na jani la juu halionekani.Lakini pia niligundua kuwa kila sehemu iliyoathilika pembeni yake kulikuwa na vijishimo vidogo vidogo.
Moja ya vijishimo karibu na mimea iliyoathiriwa


Baada ya kugundua tatizo  tulilonalo wenyeji wangu walibaini kuwa mdudu anaetusumbua ni mdudu aitwae KIYENZE....mdudu huyu hakuweza kuuawa na madawa tuliyokuwa tukitumia kwenye mimea yetu hivyo ilitubidi tufanye njia mbadala ili tuweze kudhibiti tatizo.Ilitubidi tuchimbe kila sehemu tulipoona kuna vijishimo vidogo na sehemu kubwa tulifanikiwa kuwatoa hao VIYENZE na pia tulikuta mimea mingi imekatwa na kuhifadhiwa kwenye mashimo na hao viyenze.

Baada ya tatizo hilo kujitokeza tuligundua umuhimu wa kupanda mbegu mbilimbili mpaka tatu kwenye eneo moja kwa vile sehemu ilipokatwa mche mmoja basi mche mwingine ulibaki na shughuli yetu iliendelea kama kawaida.Lakini pia nilijifunza kuwa mdudu huyu unaweza kumdhibiti katika hatua za awali kabisa kabla hajaanza kuleta madhara kwenye mimea yako kwa vile uwepo wake unapambanuliwa na vijishimo vidogo vidogo kama nilivyoonesha kwenye picha hapo juu..

Sunday 24 January 2016

NILIPOFANYA KILIMO CHA MATIKITI MAJI KWA MARA YA KWANZA. Na yohana maduhu

SEHEMU YA PILI

Hatua ya kwanza

baada ya siku nne mpaka tano mbegu zetu zilianza kumea,hivyo kazi kubwa iliyokuwepo ni umwagiliaji.tulimwagilia mala mbili kwa siku japo sio vibaya ukimwagilia maji mengi mara moja kwa siku

KAZI TU!!....
Hatua hii ya umwagiliaji iliibua changamoto kadhaa wa kadhaa ikiwamo ya kazi ngumu yenyewe ya umwagiliaji hasa kutokana na ukubwa wa shamba na vitendea kazi duni.Tulikuwa tukivuta maji kwa waterpump kutoka kwenye mto uliokuwa umbali wa mita 100 mpaka shambani kwetu tulipokuwa tumeandaa bwawa kwa ajiri ya kuhifadhia maji.Kutoka kwenye bwawa letu tulichota maji kwa kutumia ndoo kwa ajiri ya umwagiliaji.
                                       
                          Picha ya juu na chini zinaonesha tukiandaa mashine
                                kwa ajili ya kuvuta maji kutoka kwenye mto
                                     kuelekea kwenye bwawa la shambani
                            Maji kutokea mtoni yakiingia kwenye bwawa letu
                           Kijana akichota maji tayari kwa umwagiliaji wa mazao

                                      Vijana wakiwa bize kumwagilia tikitimaji...